Machapisho

Inaonyesha machapisho kuanzia Julai, 2020

NIKUSAMEHE UKAE WAPI?

Picha
Picha: 123rf. Nakumbuka siku zile, makuzi 'kinifanyia Kijijini kwenu kule, kwenu ulikokulia Sitokulaumu vile, mandhari ulozukia Nikusamehe ukae wapi, na moyo wangu uliuchana? Uliniona mdogo, kamwe sikutoshelezi Ikakujaa mikogo, kunionyesha ushenzi Na kumshika pembe mbogo, kwenye sehemu telezi Nikusamehe ukae wapi, na moyo wangu uliuchana? Ulidhani kuniacha, utaua nyota yangu Kama ndimu umechacha, watafuta namba yangu Kucha zako ulificha, ukadunga moyo wangu Nikusamehe ukae wapi, na moyo wangu uliuchana? Uliacha ngalawa, kisa muogeleaji Kila siku ulilewa, ukavujisha mfereji Ulijaa na kukupwa, kama ya bahari maji Nikusamehe ukae wapi, na moyo wangu uliuchana? Hivi sasa sikutaki, katafute kifu yako Atayekupa malaki, ufurahi nafsi yako Peke yangu nitabaki, si lazima penzi lako Nikusamehe ukae wapi, na moyo wangu uliuchana?