NIKUSAMEHE UKAE WAPI?

Picha: 123rf.

Nakumbuka siku zile, makuzi 'kinifanyia
Kijijini kwenu kule, kwenu ulikokulia
Sitokulaumu vile, mandhari ulozukia
Nikusamehe ukae wapi, na moyo wangu uliuchana?

Uliniona mdogo, kamwe sikutoshelezi
Ikakujaa mikogo, kunionyesha ushenzi
Na kumshika pembe mbogo, kwenye sehemu telezi
Nikusamehe ukae wapi, na moyo wangu uliuchana?

Ulidhani kuniacha, utaua nyota yangu
Kama ndimu umechacha, watafuta namba yangu
Kucha zako ulificha, ukadunga moyo wangu
Nikusamehe ukae wapi, na moyo wangu uliuchana?

Uliacha ngalawa, kisa muogeleaji
Kila siku ulilewa, ukavujisha mfereji
Ulijaa na kukupwa, kama ya bahari maji
Nikusamehe ukae wapi, na moyo wangu uliuchana?

Hivi sasa sikutaki, katafute kifu yako
Atayekupa malaki, ufurahi nafsi yako
Peke yangu nitabaki, si lazima penzi lako
Nikusamehe ukae wapi, na moyo wangu uliuchana?

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MPENZI BORA.